Ticker

6/recent/ticker-posts

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SEHEMU YA BAJETI YA WIZARA YA UCHUKUZI (USAFIRI NA UCHUKUZI KWA NJIA YA ANGA ) - 2015/2016

Ifuatayo ni sehemu ya bajeti ya wizara ya uchukuzi kwa upande wa usafiri na uchukuzi kwa njia ya anga kwa mwaka 2015/2016 kama ilivyowasilishwa na waziri Samueli Sitta katika bunge la bajeti mjini Dodoma.



4.0 USAFIRI NA UCHUKUZI KWA NJIA YA ANGA

4.1 Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga

90. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imeendelea kuhakikisha kuwa viwanja vya ndege na huduma za usafiri wa anga nchini vinakidhi masharti na kanuni zilizowekwa. Ili kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinazingatiwa, katika mwaka 2014/2015, viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA), Abeid Amani Karume na Kilimanjaro (KIA) vilikaguliwa na kupata vyeti vya ubora kulingana na matakwa ya vigezo vya Kimataifa ya viwanja vya ndege. Aidha, viwanja vya ndege vya Arusha, Mwanza, Kigoma, Tabora, Bukoba, Mtwara, Tanga, Lindi na Iringa pia vilikaguliwa na kupewa vyeti vya ubora. Utekelezaji wa uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini ni mzuri kiwango cha kukidhi matakwa ya Kimataifa.


91. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2014 hadi Aprili, 2015, ndege 9 ziliandikishwa kwa mara ya kwanza nchini na kupewa vyeti vya ubora. Aidha, ndege 5 zilirudishwa zilikokodishwa baada ya kumalizika muda wa mikataba ya ukodishaji. Ndege zilizorudishwa zilikuwa zikimilikiwa na Kampuni za Coastal Travellers, Zenith Aviation na Fastjet. Pamoja na kurudishwa kwa ndege hizo, Kampuni hizo zilileta ndege nyingine ili kukidhi matakwa ya utoaji wa huduma za usafiri wa anga nchini.


92. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za usafiri wa anga nchini ili kuvutia wawekezaji kutoka katika sekta binafsi au kwa ubia kati ya sekta ya Umma na sekta binafsi. Katika mwaka 2014/2015, Kampuni za ndege mpya 5 zilisajiliwa nchini ili kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga. Hatua hii inafanya Kampuni za ndege zenye leseni ya kutoa huduma za usafiri wa anga nchini kuwa 49 ikilinganishwa na Kampuni 44 zilizokuwa zimesajiliwa mwaka 2013/2014.


93. Mheshimiwa Spika, kuhusu Mikataba ya Usafiri wa Anga kati ya Tanzania na nchi nyingine (Bilateral Air Services Agreements – BASA), Wizara imeendelea kufanya mazungumzo na nchi mbalimbali ili kuipitia upya mikataba iliyopo au kuingia mikataba mipya. Lengo la kupitia upya mikataba hiyo ni kuhakikisha kuwa inakidhi mahitaji ya soko na hali halisi ya maendeleo na mabadiliko ya uchumi Duniani. Katika kipindi cha Julai, 2014 hadi Aprili, 2015, mikataba kati ya Tanzania na nchi za Zambia, Italia na Mauritius ilipitiwa upya. Aidha, Tanzania iliingia mikataba mipya na nchi za Luxemburg, Canada na Austria.


94. Mheshimiwa Spika, kutokana na uingiaji wa mikataba mipya ya BASA, hadi Aprili, 2015, Tanzania ilikuwa imeingia mikataba ya BASA na nchi 54 ikilinganishwa na nchi 50 zilizokuwa na makubaliano ya BASA na Tanzania katika kipindi kama hicho mwaka 2013/2014. Kati ya mikataba hiyo, mikataba 22 ndiyo ambayo Kampuni au mashirika yake ya ndege yanatoa huduma kati ya Tanzania na nchi husika. Kwa sasa mashirika ya ndege yanayotoa huduma za usafiri wa anga kwa utaratibu wa BASA ni 27. Nchi nyingine bado ziko katika taratibu za kuanza kutekeleza mikataba hiyo. Aidha, katika kipindi cha Julai, 2014 hadi Aprili, 2015, safari za ndege kati ya Tanzania na nchi zilizosaini makubaliano ya BASA zilikuwa 175 kwa juma. Kutokana na ukuaji wa sekta ya utalii na ongezeko la uwekezaji hususan katika sekta za Nishati na Madini na Ujenzi wa Nyumba (Real Estates), inatarajiwa kuwa hadi Juni, 2015, safari za ndege zitakuwa 213 kwa juma.


95. Mheshimiwa Spika, pamoja na mashirika ya nchi nyingi zilizosaini mikataba ya BASA kufanya safari kuanzia katika nchi zao, Mashirika mapya ya Fly Dubai na Air Seychelles ndiyo yanatoa huduma za kimataifa kuanzia nchini mwetu. Nayapongeza mashirika haya kwa kuleta changamoto kubwa katika mashirika ya ndani yanayotoa huduma za usafiri wa anga hususan ATCL, Precision na Fastjet.


96. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2014 hadi Aprili, 2015, idadi ya abiria waliotumia usafiri wa anga iliongezeka na kufikia abiria 3,852,413 ikilinganishwa na abiria 3,084,830 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2013/2014. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia abiria 4,894,328 ifikapo Juni, 2015. Idadi ya abiria waliosafiri kwenda na kutoka nje ya nchi inategemewa kuongezeka kutoka abiria 1,945,961 mwaka 2014/2015 na kufikia abiria 1,988,772 katika mwaka 2015/2016. Hili ni ongezeko la asilimia 2.2. Aidha, idadi ya abiria wa ndani inatarajiwa kuongezeka kutoka abiria 2,948,367 katika mwaka 2014/2015 hadi kufikia abiria 3,128,218 mwaka 2015/2016. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 6.1.


97. Mheshimiwa Spika, kuhusu safari za ndege (aircraft movements), katika mwaka 2014/2015, jumla ya safari za ndege 245,604 zilifanyika ikilinganishwa na safari 238,760 za mwaka 2013/2014. Hili likiwa ni ongezeko la asilimia 2.8. Kati ya safari hizi, safari za kimataifa ziliongezeka kutoka safari 39,910 mwaka 2013/2014 hadi kufikia safari 40,789 mwaka 2014/2015, sawa na ongezeko la asilimia 2.2. Safari za humu nchini pia ziliongezeka kutoka safari 198,850 mwaka 2013/2014 hadi kufikia safari 204,815 mwaka 2014/2015, sawa na ongezeko la asilimia 3.


98. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, mizigo iliyosafirishwa kwenda na kutoka nje ya nchi ilifikia tani 30,838 ikilinganishwa na tani 29,918 zilizosafirishwa mwaka 2013/14. Hili ni ongezeko la asilimia 3. Takwimu hizi zinaonesha ukuaji wa sekta ndogo ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya anga.


99. Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini imeonesha kuendelea kuimarika ambapo ukuaji wake kwa kiasi kikubwa umechangiwa na ukuaji wa uchumi wa ndani na nje ya nchi. Sababu nyingine zilizochangia katika ukuaji huo ni pamoja na kuongezeka kwa utalii nchini; kuongezeka kwa safari za ndege katika kiwanja cha ndege cha Songwe na kukarabatiwa kwa viwanja vya ndege. Aidha, kusainiwa kwa mikataba ya BASA kati ya Tanzania na nchi nyingine; mashirika ya ndege ya Emirates, Royal Dutch Airline (KLM) na Qatar Airways kuongeza safari zao za ndege na mashirika mapya ya ndege kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga kimataifa pia zimechangia katika ukuaji wa utoaji wa huduma za usafiri wa anga nchini.


100. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TCAA imeendelea kuhakikisha kuwa matukio na ajali katika usafiri wa anga zinapungua. Katika kipindi cha Julai, 2014 hadi Aprili, 2015, matukio 4 na ajali 2 za ndege zilitokea. Ajali hizi zilisababisha vifo vya watu 4 na ndege zote kuharibika kabisa. Uchunguzi wa vyanzo vya ajali zote mbili bado unaendelea.


101. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Usafiri wa Anga kwa sasa inaendelea na matayarisho ya ukaguzi wa usalama wa anga (ICAO Universal Security Audit Programme-USAP) ambao umepangwa kufanyika Septemba, 2015. Aidha, upungufu uliobainika katika ukaguzi wa Septemba, 2014 kwenye viwanja vya ndege vya JNIA na Abeid Aman Karume unaendelea kufanyiwa kazi.


102. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya mwaka 2014/2015, Serikali iliahidi kuanza kushughulikia suala la kutenganisha majukumu ya udhibiti wa usafiri wa anga na utoaji huduma ya uongozaji wa ndege. Napenda kutoa taarifa kuwa, Mtaalam Mwelekezi atakayefanya kazi ya uchambuzi yakinifu wa utenganishaji wa majukumu hayo mawili anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Juni, 2015.


103. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara ilipanga kununua rada mpya 2 za kuongozea ndege za kiraia. Taratibu za ununuzi wa rada hizo zinaendelea ambapo nyaraka za aina ya rada hizo (specifications) zimewasilishwa ICAO kwa ajili ya kuidhinishwa. Kufungwa kwa rada hizi mpya kutaendelea kulifanya anga la Tanzania kuwa salama zaidi.


104. Mheshimiwa Spika, mpango wa kubadilisha mfumo wa mawasiliano ya anga kutoka mfumo unaotumika sasa wa kutumia vituo katika viwanja vya ndege kwenda mfumo wa mawasiliano wa dijitali unaofuatilia safari za ndege unaendelea kutekelezwa. Kazi ya kubadilisha mfumo huo katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro, Songwe, Mwanza, Tanga, Tabora, Iringa na Arusha imekamilika. Kazi ya kubadilisha mfumo katika viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea na Kigoma inatarajiwa kukamilika Juni, 2015. Mfumo huu mpya utapunguza gharama za mawasiliano na kuleta uhakika wa mawasiliano baina ya vituo vya kuongozea ndege.


105. Mheshimiwa Spika, kazi ya kufunga mtambo wa kuboresha mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani wakiwa angani (VHF area cover relay station) katika kituo cha Mnyusi, Tanga imekamilika kama ilivyoahidiwa katika Hotuba ya mwaka 2014/2015.


106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara iliahidi kuendelea kulifanya anga la Tanzania kuwa salama katika usafiri wa anga. Napenda kulieleza Bunge hili kuwa, mradi wa kufunga mitambo ya ufuatiliaji wa mwenendo wa ndege angani (Automatic Dependence Surveillance – Broadcast - ADS-B) unaendelea vizuri. Mitambo hii husaidia ufuatiliaji wa mienendo ya ndege angani na hivyo kutoa fursa ya kuongoza ndege kwa uhakika na salama katika anga husika. Awamu ya kwanza ya ufungaji wa mitambo hii itakayohusu upande wa Mashariki hadi juu ya bahari ya Hindi inatarajiwa kukamilika Juni, 2015.


107. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya mwaka 2014/2015, ilitolewa taarifa kuwa Mfuko wa Mafunzo ya Marubani na Wahandisi wa Ndege ulianza kutumika kwa kufadhili wanafunzi 5 katika mafunzo ya urubani. Napenda kulieleza Bunge hili kuwa utekelezaji wa malengo ya Mfuko huu unaendelea vizuri. Aidha, wanafunzi 4 kati ya 5 walioenda mafunzoni wamehitimu mafunzo yao. Kampuni ya ndege ya Precision Air iliwaajiri vijana hao na kuwapeleka kwenye mafunzo zaidi ya aina ya ndege wanazotumia (type rating). Lengo la Mfuko huu ni kuziba pengo la uhaba wa marubani na wahandisi wa ndege unaoikabili nchi.

4.2 Huduma za Viwanja vya Ndege

108. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege iliendelea na majukumu yake ya kuhudumia na kuboresha miundombinu na huduma za viwanja vya ndege nchini. Viwanja hivyo vimeendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali ili kuwezesha ndege kutua na kuruka kwa usalama. Aidha, viwanja hivyo vilifanyiwa ukarabati wa miundombinu na uboreshaji wa mitambo.

109. Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la Tatu la Abiria (Terminal III Building) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) inaendelea vizuri. Kazi zinazoendelea ni ufungaji wa vyuma vya paa na ujenzi wa maegesho ya ndege na magari. Kazi za ujenzi wa jengo hili zinatarajiwa kukamilika Mei, 2016. Wizara inaendelea kutafuta fedha ili kuendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa jengo hilo. Kukamilika kwa awamu zote mbili kutawezesha jengo hili kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka.


110. Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kimeendelea kuboreshwa ili kuchangia katika ukuaji wa biashara za maua, mbogamboga, matunda na utalii. Katika mwaka 2014/2015, kazi za ukarabati na upanuzi wa kiwanja hiki ili kiweze kuhudumia ndege 20 kutoka 10 za sasa kwa saa ziliendelea. Mkataba wa kuanza kazi za ukarabati na upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, barabara za viungio, jengo la abiria, ujenzi wa barabara mpya ya kiungio, usimikaji wa taa za kuongozea ndege na ujenzi wa mfumo mpya wa maji taka ulisainiwa Machi, 2015. Kazi za ukarabati zinatarajiwa kuanza Juni, 2015.


111. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inaendelea na kazi za kuboresha kiwanja cha ndege cha Mwanza. Kazi zilizotekelezwa katika mwaka 2014/2015 ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa jengo la kuongozea ndege (control tower) ambapo ujenzi umefikia hatua ya control cabin; ujenzi wa jengo la mizigo umefikia hatua ya super structure na uwekaji wa tabaka la kwanza la lami katika barabara inayorefushwa ya kuruka na kutua ndege. Kazi zingine zinazoendelea ni ujenzi wa tabaka la mwisho la lami kwenye maegesho ya ndege za abiria na maegesho ya ndege za mizigo na Viungio vyake.


112. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya mwaka 2014/2015 tuliahidi kukamilisha ujenzi wa maegesho ya ndege na jengo la abiria katika kiwanja cha ndege cha Songwe. Kazi zilizofanyika ni pamoja na kukamilisha maegesho ya ndege; kuendelea na ujenzi wa jengo la abiria pamoja na barabara ya kuunganisha (by pass road) kijiji cha Iweleje na barabara kuu ya Mbeya – Tunduma; ununuzi wa gari la pili la zimamoto; usimikaji wa kamera za usalama (CCTV) na ununuzi wa mitambo maalum kwa ajili ya huduma kwa abiria na mizigo.


113. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inaendelea na kazi ya kukarabati kiwanja cha ndege cha Bukoba kwa kiwango cha lami. Katika mwaka 2014/2015, kazi za ujenzi wa barabara ya kuingia kiwanjani na maegesho ya magari kwa kiwango cha lami zilikamilika. Kazi zinazoendelea ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa jengo jipya la abiria, ufungaji mifumo ya maji safi na taka, ufungaji umeme, usimikaji wa kaunta za kisasa za kuhudumia abiria na uwekaji wa mikanda ya kusogezea mizigo. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Juni, 2015.


114. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya pili ya kazi za ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Kigoma na Tabora kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) yaliendelea na zabuni zinatarajiwa kutangazwa Julai, 2015. Aidha, taarifa za uchambuzi wa zabuni za kazi za ukarabati wa maegesho ya ndege na ujenzi wa uzio wa usalama wa viwanja hivyo zimewasilishwa Benki ya Dunia ili kupata ridhaa (No Objection). Kazi za awamu ya pili zitahusisha ukarabati wa barabara ya pili ya kutua na kuruka ndege, barabara ya kiungio na maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami; ujenzi wa uzio wa usalama; usimikaji wa taa (AGL) na mitambo ya kuongozea ndege aina ya DME na VOR.


115. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, TAA ilipanga kuanza ujenzi wa jengo jipya la abiria, maegesho ya magari, ukarabati wa barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani pamoja na kituo cha umeme katika kiwanja cha ndege cha Mafia. Kazi hizo hazikuweza kutekelezwa kutokana na uhaba wa fedha.


116. Mheshimiwa Spika, kazi ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege kumi na moja (11) vya Lake Manyara, Musoma, Iringa, Tanga, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Simiyu na Singida kwa kiwango cha lami inaendelea na itakamilika Juni, 2015. Hatua hii itawezesha kuendelea na majadiliano na Taasisi za kifedha kwa ajili ya kuanza ujenzi na upanuzi wa viwanja hivyo.

117. Mheshimiwa Spika, zabuni kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga chini ya ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya yamekamilika na kuwasilishwa Benki ili kupata ridhaa. Zabuni hizi zinatarajiwa kutangazwa Julai, 2015 na kazi za ukarabati na upanuzi kuanza Oktoba, 2015. Kazi zitakazofanyika katika viwanja hivyo ni upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege, barabara za viungio na maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami; ujenzi wa majengo ya abiria, maegesho ya magari; barabara za kuingia viwanjani na usimikaji wa taa (AGL) na mitambo ya kuongozea ndege aina ya DME na VOR.


118. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, kazi za kufanya matengenezo ya kawaida ili kuruhusu ndege kuruka na kutua kwa usalama katika kiwanja cha ndege cha Mtwara ziliendelea kutekelezwa. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuboresha na kupanua kiwanja hiki kwa kiwango cha lami. Aidha, Wizara inaendelea kufanya mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kupata fedha za kugharamia usanifu wa kina wa miundombinu na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato kwa kiwango cha lami.

119. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Wizara kupitia TAA kwa kushirikiana na Hazina, imeanza mazungumzo na Serikali ya Canada kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato kupitia Shirika la Biashara la Serikali ya Canada (Canadian Commercial Corporation - CCC). Kwa sehemu kubwa mapendekezo ya mpango wa upatikanaji wa fedha kati ya Hazina na CCC kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu na pia kwa upande wa masuala ya kiufundi kati ya CCC na TAA; yamefikiwa. Ni matarajio yetu ujenzi wa uwanja huo utaanza mwaka 2015/2016.


120. Mheshimiwa Spika, kiwanja cha ndege cha Arusha ni muhimu katika ukuaji wa sekta ya utalii nchini. Ili kuhakikisha kuwa fursa hii inatumika kikamilifu, Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inaendelea na maandalizi ya ukarabati wa kiwanja hiki. Zabuni ya kumpata Mshauri Mwelekezi wa kufanya marejeo ya usanifu wa miundombinu ya kiwanja pamoja na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya Mkandarasi zilifunguliwa Machi, 2015. Kazi ya uchambuzi wa zabuni hizi inaendelea.

121. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuboresha huduma na usalama wa viwanja vya ndege nchini katika viwango vya Kimataifa, katika mwaka 2014/2015, Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imenunua mitambo mipya minne (4) ya kufua umeme na madaraja matano (5) mapya ya kupandia na kushuka abiria (aerobridges) katika kiwanja cha JNIA. Kazi ya usimikaji wa mitambo hiyo inaendelea. Aidha, kazi ya kusimika kamera za usalama katika viwanja vya ndege vya Songwe na Arusha imekamilika na kazi za usimikaji na uboreshaji wa kamera za usalama katika viwanja vya ndege vya JNIA na Mwanza zinaendelea. Vilevile, Mamlaka ilisimika mitambo kumi (10) yenye mifumo ya teknolojia ya kisasa ya ukaguzi wa abiria na mizigo ili kuimarisha ulinzi na usalama wa usafiri wa anga katika viwanja vya JNIA (4), Songwe (2), Mwanza (1), Dodoma (1) na Bukoba (2).


122. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ilianza kazi ya kufunga mashine za kisasa za ukaguzi wa mizigo zenye uwezo wa kutambua madawa ya kulevya (rapscan x-ray machines 600 series) katika viwanja vya ndege vya Kilimanjaro, Mwanza, Songwe na Arusha.

123. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Mamlaka ilikamilisha kazi za kupima maeneo ya viwanja vipya vya ndege vya Kisumba (Rukwa), Msalato (Dodoma), Omukajunguti (Kagera) na Igegu (Simiyu). Kazi inayoendelea ni ufuatiliaji wa upatikanaji wa hati miliki ya ardhi kwa maeneo hayo.

4.3 Huduma za Usafiri wa Ndege

124. Mheshimiwa Spika, huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi ziliendelea kutolewa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na Kampuni binafsi zikiwemo Precision Air, Fastjet, Auric na Coastal Air. ATCL iliendelea kutoa huduma zake katika mikoa ya Mtwara na Kigoma na katika nchi za Burundi na Comoro kwa kutumia ndege yake aina ya Dash 8 Q300 na ndege ya kukodi aina ya CRJ-100.

125. Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zinazoikabili ATCL, Kampuni hii iliendelea kutoa huduma za usafirishaji wa abiria. Katika kipindi cha Julai, 2014 hadi Aprili, 2015, ATCL ilisafirisha abiria 40,090 ikilinganishwa na abiria 41,589 waliosafirishwa katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014. Hii ni sawa na upungufu wa asilimia 4. Sababu za upungufu huo ni pamoja na ndege aina ya Dash 8 Q300 kuwa kwenye matengenezo makubwa (C-Check). Hivi sasa huduma za usafiri wa ndege zinatolewa kwa kutumia ndege moja ya kukodi aina ya CRJ - 100.

126. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Kampuni ya ATCL imeendelea kuimarisha Chuo chake cha Air Tanzania Training Institute ili kuongeza idadi ya watoa huduma za ndani ya ndege nchini. Hadi Aprili, 2014, Chuo kimetoa wahitimu 567. Kati ya hao, asilimia 30 ya wahitimu wamepata ajira katika mashirika ya ndege ya Precision Air, Fastjet, Tropical Air na Kahama Gold Mining. Kampuni nyingi binafsi zimeoneka kuvutiwa na wafanyakazi wenye vibali au uzoefu wa fani mbalimbali. Chuo kimekuwa kikiwapatia wahitimu wake mafunzo katika fani zao na kutoa mafunzo ya kompyuta hivyo kuwa kivutio kwa waajiri. Hatua hii imesaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania.

127. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) umeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kutumia ndege nne (4) kutoa huduma za usafiri wa anga kwa Viongozi Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Katika mwaka 2014/2015, Wakala uliendelea kuzifanyia matengenezo stahiki ndege zake kulingana na sheria za usalama wa usafiri wa anga na kutoa mafunzo kwa marubani na wahandisi wa ndege zake. Aidha, Wakala uliajiri marubani wanne (wanawake wawili na wanaume wawili). Vilevile jumla ya marubani sita, wahandisi na mafundi Sanifu nane walipatiwa mafunzo.

5.0 HUDUMA ZA HALI YA HEWA

128. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) iliendelea kuboresha huduma zake katika maeneo mbalimbali. Maeneo hayo yalihusu utoaji wa huduma, vifaa, utaalam na ushirikiano. Aidha, Mamlaka ilitoa tahadhari juu ya matukio ya hali mbaya ya hewa kwa ajili ya usalama wa watu na mali zao.

129. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha utabiri wa hali ya hewa na utoaji wa tahadhari ya hali mbaya ya hewa nchini ili kuongeza ufanisi katika shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika Ziwa Victoria, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kazi ya ufungaji wa rada ya hali ya hewa huko Kiseke, Mwanza ilikamilika Desemba, 2014. Hii ni rada ya pili kufungwa nchini baada ya rada ya kwanza kufungwa Dar es Salaam mwaka

2011. Aidha, ukarabati wa ofisi za kutoa taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji walio katika maeneo ya Ziwa Victoria, Mwanza na Ziwa Tanganyika, Kigoma umekamilika na huduma zimeanza kutolewa kupitia Bandari ya Mwanza. Maandalizi ya kutoa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji walio katika maeneo ya Ziwa Tanganyika na Nyasa yanaendelea.

130. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, kupitia miradi ya mabadiliko ya tabia nchi na kupunguza athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa, Mamlaka ilinunua mitambo mitano (5) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe (Automatic Weather Stations). Hatua hii imefanya mitambo ya aina hiyo kufikia 25 nchi nzima ikilinganishwa na hitaji la mitambo 80. Aidha, Mamlaka ilifufua kituo cha kupima hali ya hewa ya anga ya juu (upper air station) huko Tabora. Ufufuaji wa kituo hiki umefanya kuwa na vituo viwili vya aina hiyo nchini ikilinganishwa na hitaji la vituo vinne. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa kuanza ujenzi wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa Hali ya Hewa imekamilika. Kazi ya usanifu wa kina inaendelea na inatarajiwa kukamilika Septemba, 2015. Aidha, Mamlaka inaendelea na taratibu za kukarabati ofisi ya Zanzibar ili kuboresha huduma za hali ya hewa. Kazi ya uboreshaji wa mfumo wa mawasiliano na uchambuzi wa takwimu za hali ya hewa katika vituo vya JNIA, Zanzibar, KIA, Mwanza na Kituo Kikuu cha Utabiri kilichopo katika Ofisi za Mamlaka zilizoko Ubungo, Dar es Salaam ilikamilika Januari, 2015.

131. Mheshimiwa Spika, Mamlaka imeendelea kuboresha uangazi wa hali ya hewa katika Bahari ya Hindi kwa kuanza kutumia maboya maalum ya kupima hali ya hewa. Aidha, maandalizi ya utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Ziwa Victoria zilikamilika. Maandalizi ya kutoa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Ziwa Tanganyika na Nyasa yanaendelea. Aidha, uboreshaji wa mfumo wa mawasiliano na uchambuzi wa data za hali ya hewa katika vituo vya JNIA, Zanzibar, KIA, Mwanza na Kituo Kikuu cha Utabiri ulikamilika Januari, 2015.

134. Mheshimiwa Spika, Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa imeendelea kujijengea heshima Kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa. Katika mwaka 2014/2015, Mamlaka ilizisaidia nchi za Saudi Arabia, Nigeria, Libya, Uganda, Burundi na Rwanda ili kuboresha shughuli za hali ya hewa kwa kutoa utaalam wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia uanzishwaji wa mfumo wa usimamizi wa utoaji huduma bora za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga na utumiaji wa mifumo ya kisasa ya utabiri wa hali ya hewa. Mashirikiano haya yameendelea kuiongezea nchi yetu heshima.

6.3 Chuo cha Usafiri wa Anga Dar es Salaam (CATC)

143. Mheshimiwa Spika, Chuo cha Usafiri wa Anga (Civil Aviation Training Centre - CATC) kimeendelea kutoa mafunzo yanayokidhi viwango vya Kimataifa katika sekta ya usafiri wa anga kwa Watanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Uganda na Rwanda. Mafunzo yanayotolewa ni ya fani za uongozaji ndege, mawasiliano, usambazaji wa taarifa za safari za ndege, usalama wa viwanja vya ndege na utafiti na ushauri kuhusu usalama wa usafiri wa anga.

144. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, jumla ya wanafunzi 531 walihitimu mafunzo. Kati yao wanafunzi 421 ni Watanzania na 110 ni kutoka nje ya nchi. Aidha, Chuo kimeanza kushirikiana na vyuo vingine vya ndani na nje ya nchi na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) ili kubadilishana mbinu na ujuzi katika uendeshaji wa mafunzo na kozi mbalimbali.
145. Mheshimiwa Spika, Oktoba, 2014, Chuo kiliandaa Mkutano Mkuu wa kwanza wa Shirikisho la Vyuo vya Usafiri wa Anga Barani Afrika (Africa Aviation Training Organization - AATO). Mkutano huo ulikuwa ni fursa nyingine ya kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake.



Post a Comment

0 Comments