Ripoti ya awali imebaini kuwa ajali ya ndege ya Air India iliyotokea mwezi uliopita na kusababisha vifo vya watu 260 ilisababishwa na kukatwa kwa usambazaji wa mafuta kwenda kwenye injini.
Ndege hiyo yenye usajili VT-ANB ikifanya safari
namba AI171, iliyokuwa ikielekea London ilikuwa imeondoka tu kwenye uwanja wa
ndege wa Ahmedabad nchini India iliposhuka ghafla na kugonga majengo ya hosteli
ya BJ Medical College, kisha kulipuka na kusambaratika huku mabawa, injini, magurudumu
na sehemu nyingine zilitawanyika kwenye eneo hilo. Watu 241 waliokuwemo ndani
ya ndege walifariki dunia, isipokuwa abiria mmoja tu aliyenusurika, na watu wengine
19 waliokuwepo ardhini waliuwawa pia.
Kwa
mujibu wa ripoti ya Shirika la Uchunguzi wa Ajali za Ndege la India (AAIB), swichi za udhibiti wa mafuta (Fuel
Control Switches) katika chumba cha marubani wa ndege hiyo aina ya Boeing 787
Dreamliner zilikuwa zimezimwa, jambo lililosababisha injini kukosa mafuta.
Wachunguzi waliweza kupata taarifa kutoka kwenye vinasa sauti vya ndege
vinavyojulikana kama “black box,” (EAFR) zikiwemo saa 49 za data za safari na
saa mbili za mazungumzo ndani ya chumba cha marubani, ikiwa ni pamoja na
kumbukumbu za ajali hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ndege hiyo ilikuwa
imefikia mwendo wa anga wa kasi ya 180 knots wakati swichi za kukata mafuta za injini
zote mbili zilipobadilishwa kutoka nafasi ya “RUN” hadi “CUTOFF” moja baada ya
nyingine kwa tofauti ya sekunde moja tu.
“Katika
rekodi ya sauti ya marubani, rubani mmoja alisikika akiuliza kwa mshangao kwa
nini mwenzake amekata mafuta. Rubani mwenzake alijibu kuwa hakufanya hivyo,”
inasomeka ripoti hiyo.
Muda mfupi baadaye, swichi hizo zilirejeshwa kwenye nafasi zake sahihi, na
injini zilikuwa katika mchakato wa kuwashwa tena wakati ajali ilipotokea.
Katika
ndege ya 787, swichi za kukata mafuta ziko kati ya viti vya marubani wawili,
mara moja nyuma ya vishikizo vya kuongeza kasi ya ndege (throttles). Swichi
hizo zinalindwa pembeni kwa upau wa chuma na zina kifaa cha kufunga
kilichoundwa mahsusi kuzuia kukatwa kwa bahati mbaya.
“Wakati swichi za udhibiti wa mafuta
zinapohamishwa kutoka CUTOFF hadi RUN ndege ikiwa angani, kila injini ina mfumo
wa kiotomatiki wa kudhibiti kuwashwa tena na kurejesha nguvu, kwa kusimamia
mchakato wa kuwasha moto na kuingiza mafuta,” inasema ripoti hiyo.
Sekunde chache baada ya injini kujaribu kuwashwa
tena injini moja iligoma kuwaka, rubani mmoja alisikika akipaza sauti, “MAYDAY
MAYDAY MAYDAY.” Msimamizi wa mnara wa uwanja wa ndege aliita namba ya
utambulisho ya ndege hiyo, lakini hakupata majibu, na alitazama ndege
ikiporomoka kwa mbali.
Rubani mkuu wa safari hiyo alikuwa na umri wa
miaka 56 na alikuwa na zaidi ya saa 15,000 za urubani katika maisha yake.
Rubani msaidizi alikuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 32, akiwa na zaidi ya saa
3,400 za kurusha ndege.
Wachunguzi pia walibaini kuwa mipangilio ya
vifaa vilivyopatikana kwenye mabaki ya ndege ilikuwa ya kawaida kwa safari ya
kuruka. Mafuta ya ndege yalichunguzwa na kubainika kuwa ya viwango
vinavyokubalika, na hakuna dalili za idadi kubwa ya ndege wa mwituni waliokuwa
karibu na njia ya ndege hiyo.
Uzito wa ndege wakati wa kuruka ulikuwa ndani
ya viwango vinavyokubalika, na hakukuwa na “mizigo hatari” ndani ya ndege hiyo.
Wachunguzi walibaini mabawa ya ndege yalikuwa kwenye nafasi ya nyuzi tano (5
degrees), ambayo ni sahihi kwa kuruka, na swichi ya magurudumu ilikuwa kwenye
nafasi ya kushuka.
Ripoti ilisema kuwa injini ya kushoto
ilisimikwa kwenye ndege hiyo tarehe 26 Machi, na injini ya kulia ilisimikwa
tarehe 1 Mei.
Safari ya ndege ya Air India 171 ilianza
kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sardar Vallabhbhai Patel mjini Ahmedabad,
katika jimbo la Gujarat, India, tarehe 12 Juni. Boeing 787-8 Dreamliner hiyo
ilikuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa London Gatwick, Uingereza, na ilitarajiwa
kutua saa 12:25 jioni kwa saa za huko.
Air India ilisema kuwa kulikuwa na abiria na
wahudumu 242 ndani ya ndege hiyo, wakiwemo raia 169 wa India, Waingereza 53,
Wareno 7 na Mkanada 1.
Mbali na waliokuwa ndani ya ndege, watu kadhaa
waliokuwa ardhini waliuawa wakati ndege hiyo ilipogonga hosteli ya Hospitali na
Chuo cha Matibabu cha BJ.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya jumla ya watu
260, kwa mujibu wa ripoti hiyo. Baadhi ya waliokufa ardhini walikuwa
waliogongwa na ndege hiyo ilipogonga hosteli.
Air India ilikiri kupokea ripoti hiyo na
ikasema itaendelea kushirikiana na mamlaka katika uchunguzi huo.
“Air
India inatoa pole na kusimama pamoja na familia na wote walioathirika na ajali
ya AI171,” shirika hilo liliandika kwenye X siku ya Jumamosi (kwa saa za huko).
“Tunaendelea kuomboleza vifo hivyo na tumejitoa kikamilifu kutoa msaada katika
kipindi hiki kigumu.”
0 Comments